Saba wafariki baada ya meli ya mafuta kupinduka pwani ya Japan
Mabaharia saba wamefariki dunia baada ya meli ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Korea Kusini kupinduka katika pwani ya magharibi ya Japan.
Waokoaji walipata wahudumu wengine wawili - mmoja wao akiwa na fahamu, wakati hali ya mwingine haijulikani, kwa mujibu wa walinzi wa pwani wa Japan waliozungumza na BBC.
Meli ya Keoyoung Sun ilipinduka katika mkoa wa Yamaguchi baada ya wafanyakazi wake kuomba usaidizi mwendo wa saa 07:00 siku ya Jumatano (22:00 GMT Jumanne).
Msako bado unaendelea kuwatafuta mabaharia wengine wawili waliokuwa ndani ya meli hiyo.
Meli hiyo iliripotiwa kutia nanga kwa sababu ya hali ya hewa ya dhoruba. Hakuna maelezo kuhusu mizigo yake iliyopatikana mara moja.
Meli hiyo inaelezewa kama "meli ya mafuta au kemikali" kwenye tovuti za usafirishaji wa baharini.
Shughuli ya uokoaji imekuwa ikifanyika karibu na mji wa Shimonoseki kusini-magharibi mwa nchi hiyo.
Vyombo vya habari vya Japan vinaripoti kuwa wafanyakazi hao ni Pamoja na Wakorea wawili, Waindonesia wanane na raia mmoja wa China.
Upepo wenye kasi ya hadi kilomita 54 (maili 33) kwa saa ulipimwa katika eneo hilo siku ya Jumatano.
bbc

Post a Comment