Mbunge Rashid Shangazi wa Mlalo agawa tani 100 za mbegu ya ngano kwa wakulima jimboni



_Februari 25, 2024._


Mbunge wa Jimbo la Mlalo Mhe. Rashid Shangazi (MNEC) ameendelea na mpango wake mkakati wa kuinua uchumi wa wananchi wake kwa kugawa Tani 100 za mbegu ya ngano kwa wakulima wa zao hilo wa Tarafa za Mtae na Mlalo. Zoezi hili limefanyika katika Kituo cha Kuongeza Thamani ya Mazao ya Kilimo Malindi na kuhudhuria na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashari ya Lushoto Bi-Ikupa Harrison Mwasyoge na wakuu wake wa idara, Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata, Maafisa Ugani na wananchi.

Ikumbukwe kwamba Mbunge huyu ameanza kwa kampeni ya kufufua zao la Kahawa kwa kugawa Bure Miche ya kwa wakulima misimu iliyopita.

Mbegu ya ngano ni sehemu ya Tani 120 iliyowasili kutoka kwa wakala wa Mbegu *ASA* ambapo tani 20 imeelekezwa katika maeneo mengine ya Halmashauri ya Lushoto yenye majimbo mawili - Lushoto na Mlalo.

Akizungumza na Viongozi na wananchi waliokusanyika kupokea mgao huo, *Mhe. Rashid Shangazi* ameeleza kwamba anagawa mbegu hii kwa lengo la kurejesha zao la Ngano Jimboni kwake kama Mbadala wa zao la Mahindi ambalo kwa miaka ya sasa limeshindwa kuwakomboa wananchi kutokana na mabadikiko ya tabia ya nchi. Hii itainua uchumi wa wananchi na Halmashauri ya Lushoto.

Mhe. Shangazi amesema, kama taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lushoto *Bi-Ikupa Harrison Mwasyoge* ilivyoeleza, Tani 19 iliyogawiwa kwa wakulima mwaka jana imezalisha Tani 305.67, kata ya Manolo ikiongoza kwa kufanya vizuri zaidi.

Matarajio yake ni kuona Tani hizi 100 zinasimamiwa kwa utaratibu mzuri zizalishe maelfu ya tani kwani mbegu imegawiwa kwa wakati sahihi kuwahi msimu wa mvua za masika.

Ameongeza kusema Halmashauri ifanye utafiti wa mazao mengine kama Parachichi ili ukifika wakati wa kuwekeza nguvu katika zao hilo wakulima wasije wakawa wamepotezwa kwa kulima bila tija na kupata hasara.

Aidha, Mhe. Shangazi amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Lushoto kushirikiana na wataalamu wake wa Kilimo kutafiti ni mazao gani yapelekwe katika tarafa ya Umba ili nao nao wanufaike na jitihada hizi za Mbunge wao.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto *Bi-Ikupa Harrison Mwasyoge* aliyezungunza kabla, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Mlalo kwa jitihada zake kwa wananchi ambazo zinamrahisishia hata yeye kama Mkurugenzi kutatua changamoto za wananchi.

Bi-Ikupa aliyeonyesha kuridhishwa na uzalishaji kutokana na Tani 19 za msimu uliopita amewataka maafisa Ugani kwenda kusimamia kwa weledi wakulima na kuhakikisha mbegu hii inapandwa kwa wakati na kufuata taratibu zote na kuonya kwamba hatovumiliwa mkulima yeyote atakayeitumia mbegu hii kinyume na malengo, akitolea Mfano kuila badala ya kuipeleka Shambani.

DED Mwasyoge ameitumia fursa ya mkusanyiko huu kuwataka wananchi kujiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja hivi karibuni akiwakumbusha wananchi kuitumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua au  kuchaguliwa.

Aidha, amewataka kuunga mkono kampeni za Serikali za kutokomeza magonjwa kama vile Mabusha, Matende, Usubi, Malaria na magonjwa mengine.

Aidha, Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Lushoto Bwana Medeye amesema Idara imejiandaa kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuzalisha zao la Ngano.

Mathalani, amesema kama mkulima atapewa kilo 20 za mbegu hiyo atalazimika kurejesha kilo 20 wakati wa Mavuno ili kuweka uhakika wa upatikanaji wa Mbegu na kuieneza kwa wakulima wengi zaidi Bure kama inavyofanyika sasa.

Ameongeza kwamba, Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imewawezesha maafisa Ugani kwa kuwapatia vitendea kazi kama pikipiki na vifaa vya kupima Afya ya udongo, hivyo wakulima wawaone maafisa Ugani hao wapime ardhi zao na kushauriwa namna Bora ya kulima kwa tija.


No comments