BASHUNGWA AIAGIZA TBA KUSHUSHA RUNGU KWA TAASISI ZA SERIKALI NA WATUMISHI WANAODAIWA
Waziri wa Ujenzi, Innocent
Bashungwa ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuelekeza nguvu ya
ukusanyaji wa kodi ya pango na majengo kwa Wizara, Taasisi na Watumishi
waliopanga kwa Wakala huo ambao wamekuwa wakisuasua kulipa madeni hayo kwa
wakati.
Ametoa agizo hilo jijini Dodoma
katika kikao cha uwasilishaji wa madai na madeni ya TBA, ambapo amesisitiza zoezi la Awamu ya pili linaloendelea lilete matokeo mazuri zaidi ya ile ya
awali ili fedha zinazopatikana zisaidie katika utekelezaji wa miradi mingine.
“Niwapongeze kwa jitihada kubwa
mliyoifanya katika ukusanyaji wa madeni Awamu ya Kwanza, Hivyo endeleeni na
nguvu ile ile katika Awamu ya Pili, matarajio yangu nikuona madeni ya TBA yanakwisha”,
amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameitaka TBA kuhakikisha
unayaangalia kwa karibu na kuyaendeleza maeneo yake katika sehemu mbalimbali
nchini ili kuepusha migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo hayo kutokana
na uvamizi.
Aidha, Bashungwa ameutaka
uongozi wa Wizara ya Ujenzi kushirikiana kwa karibu na TBA katika ukusanyaji wa
madeni ili kuongeza ufanisi na tija katika zoezi hilo.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour, ameitaka TBA kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi na kukumbusha madeni mara kwa
mara kwa wapangaji wake ili kutolimbikiza madeni hayo na mpangaji kushindwa
kulipia kwa wakati.
Akitoa taarifa, Mtendaji Mkuu
wa TBA, Arch. Daud Kondoro, ameeleza kuwa kuanzia mwezi Julai – Disemba, 2023
Wakala huo uliajiri Dalali ambaye alianza kukusanya madeni katika mikoa ya Dar
es Salaam, Dodoma, Arusha na Tanga ambapo jumla ya takribani Shilingi Bilioni
21 zilikusanywa.
“Katika makusanyo hayo kiasi
cha Shilingi Bilioni 7 .9 kilitokana na kodi ya pango na mauzo wakati kiasi cha
Shilingi Bilioni 13 kilitokana na mapato mengine”, amefafanua Arch. Kondoro.
Tangu kuanza zoezi la
ukusanyaji wa kodi Wakala umekuwa na taratibu ya kuunda timu za kufuatilia
madeni ambazo hukutana na washitiri kuwakumbusha madeni yao na kupanga mkakati
wa kulipa.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

Post a Comment