'Nilisikia sauti ikiniambia kuwa tayari Rais Nkurunziza amefariki’
Kwa watu wengi ni jambo zito na la uchungu kupokea taarifa ya kifo cha mume, na hali hii huwa nzito zaidi mume anapokuwa rais…haya ndiyo yaliyomkuta Bi Denise Nkurunziza mjane wa Rais wa zamani wa Burundi Pierre Nkurunziza.
Mwandishi wa BBC Dinah Gahamanyi hivi karibuni alikuwa jijini Bujumbura nchini Burundi na alipata fursa ya kuzungunza na Bi Denise Nkurunziza akiwa katika ofisi ya kanisa lake, na kumueleza jinsi alivyopokea kifo cha mume wake Pierre Nkurunziza aliefariki Juni 8, 2020, na namna alivyowaeleza watoto habari ya kifo cha baba yao na jinsi anavyoendesha maisha yake kama mjane.
Kifo cha hayati Nkurunziza kilikuwa ni pigo kwa Warundi wengi, wana Afrika Mashariki na watu wengine hasa waliomfahamu, lakini kwa Bi Denise na família yake kifo hiki kilibadili maisha ya familia kwa kuacha pengo kubwa lisiloweza kusahaulika, ikizingatiwa kuwa ni kifo kilichotokea ghafla. Wakati kifo kikitangazwa, Bi Denise Nkurunziza mwenyewe alikuwa ni mgonjwa katika hospitali moja mjini Nairobi Kenya ambako alikuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.
Bw Nkurunziza alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 56 na kifo chake kiliibua maswali mengi, huku baadhi wakihoji chanzo chake.
Kulikuwa na taarifa kuwa alifariki kutokana na virusi vya Corona, lakini baadaye serikali ya Burundi ilitangaza rasmi kuwa alifariki dunia kutokana na mshuko wa moyo, baada ya kupata matibabu katika Hospitali ya Karusi nchini humo.
‘Kupokea taarifa ya kifo cha Rais Nkurunziza’
Denise Nkurunziza anasema alipokea taarifa ya kwanza kuwa Rais Pierre Nkurunziza alikuwa mgonjwa mahututi ambaye hajitambui kutoka kwa mkuu wa itifaki wa rais.
Baada ya kupokea taarifa kuhusu hali ya kiafya ya mume wake Bi Nkurunziza anasema alifanya maombi na baada ya maombi akiwa ameketi alisikia sauti iliyomwambia kuwa Rais Nkurunziza alikuwa amefariki tayari .
‘’Nilisikia sauti ikiniambia kuwa tayari Rais Nkurunziza amefariki! nikaangalia kulia!, nikaangalia kushoto! Nikaangalia kila mahali nikajiuliza sauti hii imetoka wapi?, sikuona kitu chochote, nikajua ni sauti iliyotoka kwa Roho Mtakatifu’’, aliniambia Mjane wa Nkurunziza.
Baadaye Bi Denise alipata taarifa rasmi kutoka kwa serikali kwamba Rais Nkurunziza amefariki.
''Nilipokuwa hospitalini Nairobi nilichukua muda wa kusali, wakati ule nilifanya maombi ya saa matatu bila kukoma, nikiwa sehemu moja bila kuondoka sehemu hiyo nikasali kwa saa tatu mfuluriza…nikijiombea, nikiombea watoto wangu, nikiombea kilio, nikiombea mpango mzima wa mazishi kwa ujumla''
''Ulikuwa ni wakati mgumu…kuwa mcha Mungu kulinifanya nimtegemee sana Mungu, ambaye alinipa nguvu, kumtegemea Mungu kulinifanya kwanza nijiulize kwamba, Mungu alijua kifo cha mume wangu, kwasababu ameamua kumchukua siwezi kumlaumu Mungu. Mungu aliyeacha afariki amemuona na anafahamu kuwa ndio wakati wake, labda amemlinda na mambo ambayo yangetokea baadaye, mimi nilikuwa na mtizamo huo’’, anasema Bi Denise.
Mjane huyu wa hayati Nkurunziza, anapozungumzia kifo cha mumewe huenda ukakubaliana naye kwamba imani aliyonayo ndiyo inayompa nguvu za kuzungumzia kifo cha mumewe.
Kinyume na baadhi ya wanawake wajane, Bi Denise haonekani kuwa na hisia za huzuni, majonzi, wala kudondokwa na machozi anaposimulia kuhusu kifo cha mume wake Nkurunziza.
Katika muda wote wa mazungumzo yetu, kabla ya mahojiano, wakati wa mahojiano na baada ya mahojiano, alionekana mchangamfu, mwenye uso uliojaa tabasamu, huku akimsifu Mungu kwa kumpatia nguvu na ujasiri wa kupokea na kukikubali kifo cha mumewe.
Bi Denise anawasihi wanawake wanaojipata katika hali ya ujane kama yeye kuwa wavumilivu kwani ‘’yote hayawezi kutokea bila Mungu kujua, wavumilie walee watoto’’, anasema, huku akitabasamu.
‘Watoto walivyopokea kifo cha baba yao’
Kama ilivyo kwa mzazi yeyote, haikuwa rahisi kwa Bi Denise Nkurunziza kuwafahamisha watoto wake sita wa kuzaa na wengine wengi yatima anaowalea kuhusu taarifa ya kifo cha baba yao.
‘’Halikuwa jambo rahisi kusema kweli, kuwafahamisha watoto wangu kifo cha baba yao, lakini kwa sababu nilikuwa nimewaombea na kumuomba Mungu anipe ujasiri, niliweza kuwafahamisha’’, anasema na kuongeza kuwa: ‘’ Kusema kweli ukiniuliza jinsi nilivyoweza haya yote…siwezi kukueleza, ilikuwa ni nguvu ya mwenyezi Mungu’’
‘’Baada ya kupokea taarifa ya kifo cha baba yao, nikiwa hospitalini Nairobi niliwapigia simu ya vídeo [vídeo call], nikawaambia…mnanitazama? Wakasema ndio? Nikawauliza mnaniona jinsi nilivyo? Wakasema ndio, nikawaambia si mnaniona mimi ni mwenye furaha? Wakasema ndio mama…Nikawaambia sasa ninataka kuwapa taarifa na ninataka mkiipokea muwe wenye furaha tu kama mimi wakasema ndio…Ndipo nilipowaambia baba amefariki...Niliposema hivyo tu nikaona kamera ya video inaanza kuyumba…baadhi yao wakatoka mbele ya kamera wakaenda vyumbani kulia, nikawaambia walezi wawaache walie…walilia kisha wakanyamaza’’, anakumbuka Bi Nkurunziza.
Hatahivyo anasema mmoja wa watoto yatima anaowalea hakulia wakati ule kwasababu alidhani aliyefariki ni baba yake Bi Denise Nkurunziza [babu yao].
‘’Wenzake walimuuliza ni kwanini hakulia?, akasema babu alikua amezeeka sana ndio maana sikulia, lakini baadaye alipofahamishwa vizuri alilia sana, lakini baadaye wote walinyamaza’’, anasema.
‘’Unajua watoto nyakati za vilio huwatazama wazazi wao, wakati wote wa kilio walikuwa wananitazama jinsi ninavyojichukua…kama mlifuatilia kilio cha Nkurunziza binafsi sikulia kabisa nilikua mwenye nguvu, hata wakati wa mazishi nilizungumza, wengi walijiuliza niliwezaje kupata ujasiri wa kumzungumzia mume wangu katika kilio na mazishi vile?...naweza kusema ni ‘Mungu’ aliyeniwezesha kwa hivyo watoto walifuata mfano wangu hawakulia…waliniambia mama tulikua tunakutazama wakati wote wa mazishi, ungelia tu, na sisi tungelia!’’, aliniambia Bi Nkurunziza.
‘Maisha baada ya kifo cha Nkurunziza’
Kuhusu maisha yake baada ya kifo cha mumewe Pierre Nkurunziza, Bi Denise, alisema huku akitabasamu ’’ Nimekuwa nikifanya kazi ya Mungu, nikiwa Mke wa Rais na sasa ninaendelea nayo,’’ alisema.
Bi Denise haonekani kwa sasa haonekani katika siasa za Burundi japo hayati Nkurunziza alikuwa mwanachama wa chama tawala cha CNDD/FDD? Kuhusu hilo alijibu: ‘’Hapana mimi sio mwanasiasa, mimi nina kazi ya maombi, kuwaombea wanasiasa na wanananchi kwa ujumla… unajua kama kanisa tunajukumu la kuwaombea viongozi na chama kilichopo madarakani ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, hiyo ndio kazi ninayoifanya’’, alisema.
‘’Nina vituo vya kuwalea mayatima wengi katika maeneo mbali mbali ya nchi na nimekuwa nikiwatembelea na kuwasaidia , pia ninawasaidia akinamama wajane, kwa kuwatafutia misaada mbali mbali ndio kazi ambayo nimekuwa nikiifanya’’, aliongeza.
Bi Denise pia ameeleza namna anavyoweza kuwalea watoto wengi mayatima pamoja na kuwasaidia wanawake wajane nchini Burundi. ’’Hata kabla hatujaingia Ikulu nikiishi katika mtaa wa Bwiza wakati ilikuwa shida kwangu kula nilikuwa ninaishi na watoto yatima, tulikuwa tukishiriki chakula kidogo nilichokuwa nacho…binafsi mimi nilikuwa ninasema chakula ninachokula mimi hata mtoto wa pili anaweza kula, hata watatu, hata wanne wanaweza kukila, kwangu mimi kusaidia sio lazima uwe na vitu vingi.’’
Amekanusha kuwa anapata misaada kutoka serikalini na mashirika ya kigeni kwa ajili ya kuwatunza watoto yatima anaowalea: ’’Sipati msaada wowote kutoka kwa mashirika makubwa, ni watu binafsi tu wanajitolea kuwasaidia, kwa mfano katika sherehe za Krismasi na Pasaka akinamama wengi hukusanya misaada mingi kwa ajili ya watoto yatima na kuniletea’’, alijibu.
Mjane huyu wa hayati Nkurunziza ambaye ni Mlokole tangu mwaka 1997, aliwekewa wakfu kuwa mchungaji Julai, 2011 na anamiliki Kanisa lenye uwezo wa kuwapokea waumini 10,000 mjini Bujumbura. Baada ya mahojiano na BBC alijiunga na kwaya yake kanisani iliyokuwa ikifanya mazoezi ya nyimbo na kisha kuimba nayo nyimbo za kuabudu. Bi Denise Binafsi ni muimbaji wa kwaya ya kanisa lake.
Baada ya mahojiano nilipata fursa ya kuingia katika kanisa la Bi Denise Nkurunziza ambapo niliikuta kwaya yake jukwaani, ikiwatumbuiza waumini takriban 100 hivi, waliokuwa wamefika kwa ajili ya ibada ya jioni iliyoanza baadaye.
Hakuchelewa, mara Bi Nkurunziza aliingia katika kanisa lake ambapo alisimama kando ya kwaya kwa muda wa dakika kama 10 hivi akiitazama kwaya, na kisha alipanda jukwaani kuzungumza na baadhi ya wanakwaya mmoja baada ya mwingine, huku kiongozi wa kwaya akiimba wimbo wa kuabudu.
Baada ya muda mfupi alishuka jukwaani na kuelekea kwenye kiti chake kilichopo mbele na kuanza kuimba nyimbo za kuabudu, huku akinyoosha mikono yake juu, huku akionekana kuzama ndani ya maombi, muda wa ibada ulikuwa umeanza.

 
 
Post a Comment