Kichapo cha Yanga chamtimua Kocha Robertinho Simba

 


Klabu ya Simba imemtimua kazi kocha wake mkuu Roberto Oliveira siku mbili baada ya kukubali kichapo kizito cha goli 5-1 kutoka kwa wapinzani wao wa jadi Yanga.

Kocha huyo raia wa Brazil maarufu kwa jina la Robertinho alijiunga na Simba akitokea klabu ya Vipers ya Uganda mwezi Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula, makubaliano ya kuvunja mkataba yanefikiwa na pande zote mbili, klabu na kocha mwenyewe. Simba pia imesitisha mkataba na kocha wake wa viungo Corneille Hategekimana.



Katika kipindi cha mpito klabu hiyo itanolewa na kocha wake wa makipa Daniel Cadena atakayesaidiwa na nahodha wa zamani wa klabu hiyo Selemani Matola.

Kumekuwa na manung’uniko kutoka kwa mashabiki wa klabu ya Simba toka kuanza kwa msimu juu ya mbinu za kiufundi za kocha huyo. Kipigo cha 5-1 kutoka kwa Yanga kimefanya malalamiko hayo kupaa zaidi.

Mara ya mwisho Simba kupokea kichapo kizito kama hicho kutoka kwa Yanga ilikuwa miaka 55 iliyopita.


No comments