Balozi Kingu asisitiza ubora wa vifaa na kuongeza nguvu miradi ya REA


🔹 Lengo ni kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati


Na Veronica Simba, SONGEA


Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amewaagiza Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani Songea, kuzingatia matumizi ya vifaa vyenye ubora  na kuongeza nguvu kazi ili miradi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa.

Balozi Kingu pia amewataka Wakandarasi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia usalama wa miradi wanayoitekeleza ili azma ya Serikali kuhakikisha inawanufaisha wananchi iweze kutimizwa.

Amesema hayo leo Novemba 19, 2023 alipokuwa akizungumza na Wakandarasi kutoka kampuni ya White City na Namis Corporate Ltd ambao wanatekeleza miradi ya umeme vijijini wilayani Songea.

“Nawasisitiza mtembee katika ratiba tuliyokubaliana kwani mkikamilisha miradi kwa wakati na ubora ni sifa kwenu pia na historia itaandikwa kuwa mlichangia katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati adhimu ya umeme,” amesema.

Akizungumzia takwimu za umeme vijijini kwa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, Balozi Kingu amesema jumla ya vijiji 442 kati ya 554 vimekwishafikishiwa umeme sawa na asilimia 79.8 na kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Desemba mwaka huu, vijiji vyote vitakuwa vimefikishiwa nishati hiyo.

Akidadavua zaidi, amesema kuwa kwa Wilaya ya Songea, Mkandarasi Namis Corporate Ltd alipewa vijiji 165 ambapo hadi sasa amekwishawasha vijiji 82 na ifikapo Novemba 22 atakuwa amewasha vingine 25 hivyo kufikisha vijiji 107.

“Kati ya vijiji 58 ambavyo Namis atakuwa kabakiza tumekubaliana kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu atakuwa amewasha 44 na kufikia Desemba 30 atakuwa amewasha 18 vilivyobaki hivyo kukamilisha vijiji vyote.”

Kwa upande wa Mkandarasi White City, Mwenyekiti wa Bodi ameeleza kuwa alipewa vijiji 99 na mpaka sasa amewasha vijiji 77 na kubakiwa na 22. Hata hivyo, kati ya hivyo 22 vilivyobakia, 15 vitakuwa vimewashwa ifikapo Novemba 27 na 7 ifikapo Desemba 5 mwaka huu.

No comments